By Perez Karisa, July 3, 2026
Zaidi ya watu milioni 200 nchini Marekani wamewekwa chini ya tahadhari ya joto kali baada ya kile kinachoitwa heat dome kutanda katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, kikisababisha viwango vya joto vinavyohisiwa kufikia rekodi mpya.
Kwa mujibu wa Huduma ya Kitaifa ya Hali ya Hewa (NWS), ingawa halijoto ya kawaida inakaribia nyuzi 38 za Selsiasi, unyevunyevu mkubwa umefanya joto linalohisiwa kufikia kati ya nyuzi 43 na 46 katika miji mikubwa kama Washington D.C., Philadelphia, New York na Boston.
Maafisa wa hali ya hewa wamesema hali hiyo imekuwa hatari zaidi kutokana na joto kuendelea hata usiku, ambapo halijoto haishuki chini ya nyuzi 24 hadi 27 za Selsiasi, jambo linalozuia miili ya watu na nyumba kupoa.
Wimbi hilo la joto pia limeathiri maandalizi ya maadhimisho ya miaka 250 ya Uhuru wa Marekani. Baadhi ya shughuli, ikiwemo onesho la rodeo mjini Washington D.C., zimeahirishwa huku gwaride la Philadelphia likifupishwa ili kulinda washiriki dhidi ya madhara ya joto.
Aidha, mechi kadhaa za Kombe la Dunia la FIFA zinazotarajiwa kuchezwa katika miji iliyoathirika zimechochea waandaaji kuweka mikakati maalumu ya kuwakinga mashabiki na wachezaji dhidi ya athari za joto kali.
Mahitaji makubwa ya matumizi ya viyoyozi pia yameweka shinikizo kwa gridi ya umeme, huku mamlaka zikiwataka wananchi kupunguza matumizi ya umeme ili kuepusha kukatika kwa huduma.
Mamlaka zimewahimiza wananchi kukaa katika maeneo yenye viyoyozi, kunywa maji ya kutosha, kuwajali wazee, watoto na wanyama wa kufugwa, pamoja na kuepuka shughuli nzito za nje wakati wa mchana ili kupunguza hatari ya uchovu mkali au kiharusi kinachosababishwa na joto.

