By Perez Karisa, July 3, 2026
Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga amekutana na Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata pamoja na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi mjini Kisii, katika kikao kilichofanyika nyuma ya milango iliyofungwa kuelekea mikutano ya kisiasa ya vuguvugu la Linda Mwananchi inayotarajiwa kufanyika katika kaunti za Kisii na Nyamira.
Kikao hicho kimeibua mjadala mkubwa wa kisiasa kutokana na kuwakutanisha baadhi ya viongozi wanaohusishwa na harakati za kujenga muungano mpya wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Baada ya mkutano huo, Maraga alisisitiza umuhimu wa kile alichokiita ukombozi wa taifa, akitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka tofauti zao kando na kushirikiana katika kuijenga upya Kenya kwa kuzingatia Katiba, utawala wa sheria, uwajibikaji na fursa endelevu za kiuchumi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kang’ata alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akidokeza kuwa Maraga amejiunga na kile alichokiita “Linda Kisii”, hatua iliyozua tetesi kuhusu uwezekano wa kiongozi huyo wa chama cha United Green Movement (UGM) kushirikiana rasmi na vuguvugu la Linda Mwananchi. Hata hivyo, hakukuwa na tamko rasmi lililotolewa na Maraga kuthibitisha kuwa amejiunga na muungano huo wa kisiasa.
Baada ya kikao hicho, viongozi hao walielekea kwenye ziara ya kuhamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya Kisii na Nyamira. Ziara hiyo inaongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Gavana wa Siaya James Orengo, wakisaidiwa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi pamoja na Seneta wa Kisii Richard Onyonka.
Mikutano ya hadhara imepangwa kufanyika katika maeneo ya Monarch Mosocho, Keumbu Stop, Keroka na baadaye kufungwa kwa mkutano mkubwa katika mji wa Kisii.
Kupitia mikutano hiyo, viongozi wa Linda Mwananchi wanatarajia kueleza sera zao huku wakijielekeza katika masuala ya uwajibikaji wa viongozi, kupunguza gharama ya maisha, kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuimarisha utawala wa sheria. Pia wanajinasibu kuwa ndio sauti mbadala ya upinzani inayolenga kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.
Ziara hiyo inafanyika wakati shughuli za kisiasa nchini zinaendelea kushika kasi, huku viongozi mbalimbali wakijipanga na kujenga miungano mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

