By Perez Karisa, July 3, 2026
Gavana wa Murang’a, Irungu Kang’ata, amesema kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi ndilo pekee lenye uwezo wa kuikomboa Kenya kisiasa na kiuchumi, akisisitiza kuwa lina ajenda ya kuunganisha Wakenya na kuimarisha taasisi za serikali kupitia utawala wa sheria.
Akizungumza mjini Kisii kabla ya kuanza kwa mikutano ya uhamasishaji wa wananchi katika eneo la Gusii, Kang’ata alisema Linda Mwananchi ndilo vuguvugu pekee lenye sura ya kitaifa na linalowapa nafasi Wakenya kutoka maeneo yote ya nchi kushiriki katika kujenga mustakabali wa taifa.
Alisema kuwa chini ya uongozi wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, vuguvugu hilo limejikita katika kuleta mageuzi ya kweli kupitia kuheshimu Katiba, kuimarisha uwajibikaji serikalini na kuinua uchumi wa wananchi.
Kang’ata alisema kuwa iwapo Linda Mwananchi itaunda serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, itatekeleza sera ya elimu ya bure kwa wanafunzi wote, kuanzia ngazi za chini hadi juu kulingana na mpango wake wa elimu. Pia alisema serikali hiyo itaimarisha mfumo wa afya kwa kuhakikisha Wakenya wanapata huduma bora, nafuu na zinazopatikana kwa urahisi katika hospitali za umma.
Aidha, gavana huyo aliikosoa serikali ya Rais William Ruto kuhusu ushuru wa Nyumba (Housing Levy), akisema makato hayo yanaendelea kuongeza mzigo wa maisha kwa wafanyakazi na wananchi bila kutoa manufaa yanayoonekana kwa walio wengi. Alisema serikali inapaswa kutafuta mbinu mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo badala ya kuongeza mzigo wa kodi.
Katika masuala ya haki za binadamu, Kang’ata alilaani visa vya utekaji nyara, kutoweka kwa watu kwa lazima na mauaji ya kiholela, akisema matukio hayo yanahatarisha demokrasia na haki za msingi zilizopiganiwa na mashujaa wa mageuzi kama Kenneth Matiba na Charles Rubia. Alisisitiza kuwa Kenya inapaswa kulinda uhuru wa kujieleza na kuhakikisha vyombo vya usalama vinafanya kazi kwa kuzingatia sheria.
Kang’ata pia alizungumzia hatua yake ya kujiondoa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA), akisema alifanya uamuzi huo kutokana na tofauti za kimtazamo kuhusu mwelekeo wa uongozi wa taifa. Alieleza kuwa Linda Mwananchi ni jukwaa la kisiasa lililo wazi kwa viongozi wote wenye maono ya kuleta mabadiliko, bila kujali vyama wanavyotoka.
Vilevile, alitoa wito wa ushirikiano mpana kati ya Linda Mwananchi na muungano wa upinzani unaohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Kwa mujibu wake, umoja wa vyama na viongozi wa upinzani utakuwa muhimu katika kujenga nguvu ya kisiasa itakayoweza kushindana na serikali ya sasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Kauli za Kang’ata zinajiri wakati shughuli za kisiasa nchini zinaanza kushika kasi huku viongozi mbalimbali wakijipanga mapema kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027, kupitia mikakati ya kujenga miungano mipya na kuimarisha ushawishi wao katika maeneo mbalimbali ya nchi.

